Mkoa wa Morogoro umepanga kutumia kiasi cha shilingi trilioni 1.3 kwa mwaka wa fedha 2025/2026 kati ya fedha hizo kiasi cha shilingi 946.7 Bil. kimetengwa kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo iliyopangwa kutekelezwa Mkoani humo kwa mwaka huo wa fedha.
Hayo yamebainishwa na Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Mhe. Adam Kighoma Malima, Machi 6, 2025 wakati wa kikao cha 43 cha Kamati ya Ushauri ya Mkoa (RCC) kilichofanyika Ukumbi wa Mikutano wa Magadu Manispaa ya Morogoro kikilenga kujadili mwenendo wa mpango na bajeti ya Mkoa kwa mwaka wa fedha 2025/2026.
Akifafanua zaidi, Mhe. Malima amesema kuwa kiasi cha shilingi 389.9 zitatumika kwa ajili ya mishahara ya watumishi wa umma na matumizi mengine ya kawaida.
"Katika mapendekezo ya bajeti ya mwaka 2025/2026, Mkoa wa Morogoro unakadiria kutumia jumla ya shilingi trilioni 1.3 kwa ajili ya miradi ya maendeleo na matumizi mengine ya kawaida," amesema Mhe. Malima.
Mhe. Adam Malima ametumia kikao hicho kuwakumbusha watumishi wa umma ndani ya Mkoa huo kushiriki shughuli za kijamii, ikiwa ni pamoja na maadhimisho ya Siku ya Wazee Duniani na kushiriki kikamilifu maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani yatakayofanyika kimkoa Machi 8, 2025, katika Halmashauri ya Mji wa Ifakara.
Kwa upande wake, Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe. Prof. Palamagamba Kabudi, amesisitiza umuhimu wa usimamizi mzuri wa miradi ya maendeleo, hasa ile inayogusa wananchi wa hali ya chini kama shule, zahanati na vituo vya afya.
Naye, Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Morogoro, Mhandisi Joseph Masunga, ameipongeza Serikali ya Mkoa huo kwa juhudi za kuimarisha mahusiano baina ya wakulima na wafugaji, hali iliyosaidia kupunguza migogoro ya pande hizo mbili, hata hivyo amesisitiza kuongeza jitihada katika kutatua migogoro ya ardhi kati ya wananchi na hifadhi pamoja na migogoro baina ya wananchi na taasisi za umma.
Mwisho.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Morogoro
Sanduku la Posta: S.L.P 650 MOROGORO
Simu: +2550232934305
Simu: +255766828252
Barua pepe: ras.morogoro@tamisemi.go.tz
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.