Zaidi ya shilingi Bil.347 zimetengwa kwa ajili ya kutekeleza ujenzi wa miradi mikubwa ya kitaifa Mkoani Morogoro ikiwemo mradi wa Ujenzi wa barabara ya Bigwa – Kisaki Mkoani humo.
Hayo yamebainishwa na Meneja wa TANROARDS Mkoa wa Morogoro Mhandisi Lazeck Kyamba Januari 7, Mwaka huu wakati wa kikao cha 42 cha Bodi ya Barabara kilichofanyika katika ukumbi wa Magadu uliopo Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro.
“...Mheshimiwa mwenyekiti Mkoa wa Morogoro una miradi mitano mikubwa ya kitaifa ukiwemo mradi ujenzi wa barabara ya Ifakara – Kihansi mpaka Mlimba, Taweta Madeke Sehemu ya Ifakara hadi Mbingu ..” Amesema Mhandisi Lazeck Kyamba.
Akifafanua zaidi, Mhandisi Kyamba amebainisha miradi hiyo inayoendelea kujengwa Mkoani humo ni pamoja na mradi wa barabara ya Bigwa – Kisaki wenye thamani ya Tsh. Bil 132, mradi wa barabara ya Ifakara - Kihansi – Mlimba – Taweta - Mbingu yenye thamani ya Tsh. Bil. 97.2,
Mradi mwingine ni mradi wa barabara ya Ubena Zomozi – Ngerengere itakayogharimu kiasi cha Tsh. Bil 20.5, mradi wa barabara ya Ifakara - Kihansi – Mlimba – Taweta sehemu ya Ifakara – Mbingu - Chita utagharimu kiasi cha Tsh. Bil 70.8, lakini pia mradi wa ujenzi wa barabara ya kuingia kwenye vituo vya kushushia na kupakia mizigo na abiria vya treni ya kisasa ya SGR.
Aidha, Mhandisi huyo amesema kumekuwa na uharibifu mkubwa wa miundombinu hususan makaravati, barabara na madaraja hivyo serikali ngazi Mkoa iliidhinishiwa na Serikali Kuu kiasi cha Tsh. Bil. 20.7 kwa mwaka wa fedha 2024/2025 ili kufanya matengenezo ya kudumu ya miundombinu ya barabara na bajeti ya Tsh. Bil 3.5 zikiwa fedha za miradi ya maendeleo.
Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Mhe. Adam Kighoma Malima amesema serikali imejipanga kupunguza ajali za barabarani Mkoani humo kwa kushirikiana na jeshi la polisi huku akisisitiza kujiandaa kuwekeza kwenye matumizi ya mifumo ya kidijitali ikiwemo kufunga ta ana kamera za barabarani ili kutambua makosa yanayofanywa na baadhi ya madereva wasiozingatia sheria za barabarani .
Katika hatua nyingine, Mhe. Malima amekemea vikali tabia ya baadhi ya wamiliki wa magari ambao magari yao yakiharibika yanaegeshwa barabarani na hata kufanyiwa wengine kudiliki kufanyia matengenezo ya magari hayo barabarani badala ya kuyavuta na kuyaweka mahali salama na kwamba watachukua hatua kwa wamiliki wenye tabia hiyo.
Naye, Mbunge wa Jimbo la Morogoro Kusini Mhe. Innocent Kalogeresi ameshauri Serikali iongeze bajeti ya fedha za TARURA na TANROADS Mkoani humo ili kukidhi haja ya kutengeneza miundombinu ya Mkoa huo kwa sababu ni mkoa mkubwa na unam aji mengi yanayoharibu miundombinu.
Kwa upanade wake Mbunge wa Malinnyi Mhe. Antipasi Mgungusi ameiomba Serikali kukamilisha kivuko cha Kikove ili wananchi wa Malinyi na Mlimba kupata urahisi wa kusafiri kwenda Mkoani Songea badala ya kuzunguka kupitia Mkoa wa Iringa.
Mwisho
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Morogoro
Sanduku la Posta: S.L.P 650 MOROGORO
Simu: +2550232934305
Simu: +255766828252
Barua pepe: ras.morogoro@tamisemi.go.tz
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.