Katibu Tawala wa Mkoa wa Morogoro Dkt. Mussa Ali Mussa ametoa miche 10 ya mikarafuu kwa kila mwanafunzi wa kidato cha kwanza katika shule ya Sekondari Kisemu iliyopo Halmashauri ya Wilaya ya Morogoro Mkoani humo kama ishara ya kuendeleza Kampeni ya Jisomeshe na Mkarafuu katika Mkoa huo.
Dkt. Mussa amegawa miche hiyo February 25, Mwaka huu wakati wa ziara yake ya kikazi ya kukagua miradi ya usambazaji endelevu wa maji vijijini na usafi wa mazingira (SRWSS) katika vituo vya afya vya Halmashauri ya Wilaya ya Morogoro na shule hususan ujenzi wa vyoo.
Aidha, Dkt. Mussa amewataka wataalam wa kilimo kutembelea shule hizo na kutoa Elimu ya kustawisha zao la karafuu kwa wanafunzi ili kusaidia kutunza miche ili liweze kuwa tija kwao na kwa wazazi hivyo kusaidia gharama ya watoto hao katika kupata Elimu kupitia zao hilo la karafuu.
Amesema kampeni hiyo ya JISOMESHE NA MKARAFUU inalenga wanafunzi wa kidato cha kwanza kupanda miche hiyo ili kuwanufaisha wanafunzi kwa kujisomesha wenyewe kupitia zao la karafuu na kukuza kipato cha familia zao, lakini pia kutunza mazingira katika ngazi ya Mkoa na Taifa kwa ujumla.
“…mikarafuu hii mtaweza kukaa nayo kwa miaka 4 kisha itaanza kuzaa mtakapofika kidato cha nne kabla ya kufanya mtihani basi itaanza kuzaa na kila mkarafuu utazaa sio chini ya kilo 5” amesema Dkt. Mussa
Aidha, Kampeni hiyo ni moja wapo ya hatua za utekelezaji wa ajenda ya kilimo ifikapo 2030 huku wakiendelea kukuza kipato kinachotokana na mazao ya viungo kwani mazao hayo ni mazao ya kimkakati katika Mkoa wa Morogoro ikiwemo zao la parachichi, Kakao, Mchikichiki na karafuu yenyewe.
MWISHO.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Morogoro
Sanduku la Posta: S.L.P 650 MOROGORO
Simu: +2550232934305
Simu: +255766828252
Barua pepe: ras.morogoro@tamisemi.go.tz
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.