Januari 16, 2023 Mkoa wa Morogoro umepokea ujumbe wa Maofisa wa Kijeshi kutoka Chuo cha Taifa cha Ulinzi kilichoko Jijini Dar es Salaam Maofisa hao wapo Mkoani hapa kwa ajili ya mafunzo kwa vitendo katika maeneo mbalimbali ya Mkoa huo.
Maofisa wa Jeshi kutoka Chuo cha Ulinzi cha Taifa wakisaini kitabu cha wageni mara baada ya kuwasili katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Morogoro.
Akitambulisha ujumbe huo mbele ya Katibu Tawala wa Mkoa huo Dkt. Mussa Ali Mussa, Brigedia Jenerali Stephen Mnkande ambaye pia ndiye Kiongozi wa Msafara huo amesema lengo la ujio wao ni kufanya mafunzo kwa vitendo yanayoashiria kumalizika kwa muhula wa pili wa masomo ya chuo hicho kwa mwaka 2022/2023.
Aidha, Lengo mahususi amesema ni kutaka kujifunza zaidi masuala mbalimbali ya kisiasa, kijamii, kiuchumi, kilimo na viwanda yanavyo athiri usalama katika Maeneo wanayotembelea ukiwemo Mkoa wa Morogoro.
Katibu Tawala wa Mkoa wa Morogoro Dkt. Mussa Ali Mussa wakati akiwakaribisha Maofisa hao kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Mhe. Fatma Abubakar Mwassa amesema kupitia mafunzo yao Serikali ngazi ya Mkoa itachukua mapendekezo, mawazo na ushauri wao kwa ajili ya kuboresha namna ya kutatua changamoto katika utekelezaji wa majukumu ya kiserikali.
Maofisa hao wa kijeshi walioambatana na Maofisa wengine kutoka nchi za Nigeria, China, Burundi, Rwanda na wenyeji Tanzania wanafanya ziara hii ya mafunzo wakiwa tayari wamekamirisha ziara kama hiyo Mkoani Tanga iliyofanyika kwa siku sita.
MWISHO.
Katibu Tawala Mkoa wa Morogoro Dkt. Mussa Ali Mussa akitoa zawadi ya kitabu kwa Brigedia Jenerali Stephen Mnkande, kitabu hicho wasifu wa Mkoa wa Morogoro.
Dkt. Mussa Ali Mussa Katibu Tawala Mkoa wa Morogoro akipokea zawadi ya kalenda na Nembo ya Chuo cha Ulinzi cha Taifa kutoka kwa Brigedia Jenerali Stephen Mnkande baada ya kumalizika kwa kikao kifupi katika ukumbi wa mikutano Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Morogoro.
Katibu Tawala Mkoa wa Morogoro Dkt. Mussa Ali Mussa akiwa na Sekretarieti ya Mkoa kwenye picha ya pamoja na Maofisa wa Kijeshi kutoka Chuo cha Taifa cha Ulinzi baada ya kikao kifupi katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Morogoro.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Morogoro
Sanduku la Posta: S.L.P 650 MOROGORO
Simu: +2550232934305
Simu: +255766828252
Barua pepe: ras.morogoro@tamisemi.go.tz
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.