Waziri Bashungwa akagua miradi ya maendeleo Kilosa aacha maagizo mazito
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Innocent Lugha Bashungwa amefanya ziara ya kikazi ya siku moja Wilayani Kilosa Mkoani Morogoro ziara iliyolenga kukagua miradi ya maendeleo inayotekelezwa Wilayani humo huku akiacha maagigo mazito yanayotakiwa kutekelezwa.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na serikali za Mitaa (MB) Innocent Bashungwa akiongea na wafanya biashara ndogo ndogo (hawapo pichani) wa eneo la Mtumbatu Wilayani Kilosa alipofanya ziara ya siku moja wilayani humo
Waziri Bashungwa amefanya ziara hiyo Julai 23, 2022 na kutembelea miradi mitatu ikiwemo ujenzi wa Sekondari ya Belega ambayo imepelekewa shilingi Bilioni Moja, ujenzi wa Daraja la Belega lenye Urefu wa mita 140 ambapo hadi kukamilika kwake litagharimu zaidi ya shilingi 7.9 Bil. Pamoja na Kituo cha Afya cha Nhembo ambacho nacho kimepelekewa shilingi milioni 700.
moja ya majengo ya sekondari ya Belega wilayani Kilosa ambayo Waziri Bashungwa ameyatembelea.
Akiwa katika Sekondari ya Belega amemuagiza Mkuu wa MKoa huo Martine Shigela kusimamia kamati mbili zilizoundwa kuangalia matumizi ya fedha Shilingi Bilioni Moja zilizoletwa na Serikali katika shule hiyo kwa ajili ya kidato cha tano na cha sita kama matumizi yake yamefuata taratibu na miongozi iliyopo na kumtaka kuwasilisha taarifa ya kamati hizo haraka Ofisini kwake.
“nimemuelekeza Mkuu wa Mkoa kwa utaratibu ambao tayari umeutoa, sasa lipe msukumo, timu ifike tujiridhishe kama Bilioni moja ambayo mheshimiwa Rais amewezesha wananchi wa Jimbo la Kilosa Kupitia kwa Mbunge Mhe. Profesa Kabudi kama tumepata matumizi halisi ya hiyo Bilioni moja” aliagiza Waziri Bashungwa.
Waziri wa TAMISEMI Innocent Bashungwa (wa pili kushoto) akikagua ujenzi wa majengo ya shule ya sekondari Belega Julai 23 mwaka huu. kushoto ni DED wa Halamshauri ya Wilaya ya Kilosa Kisena Mabuba na kutoka kulia ni Mkuu wa Wilaya ya Kilosa Majid Mwanga na Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Martine Shigela
Katika Hatua nyingine amemuagiza Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilosa Kisena Mabuba kuhakikisha watoto wa kidato cha tano wanaotarajia kuanza hivi karibuni kuanza kutumia vyumba vya madarasa ya shule hiyo yanayoendelea kukamilishwa sasa.
Baadhi ya wanafunzi wa Shule ya Sekondari Belega.
Akiwa katika mradi wa ujenzi wa Daraja la Berega ambalo limewakosesha wananchi wa kata ya Belega mawasiliano kwa muda mrefu na hata kusababisha vifo vya wakazi wake amemtaka mkandarasi anayejenga daraja hilo lenye urefu wa mita 140 Nyanza Road Works Ltd kukamilisha kazi hiyo ifikapo mwezi Juni 2023 kama mkataba unavyoonesha.
Hili ndo Daraja la Belega ambalo linalotumika kwa sasa, ambalo ni hatari kwa wananchi wakati wa masika.
Maagizo hayo ameyaelekeza pia kwa Meneja wa Wakala wa Barabara Mijini na Vijijini TARURA Mkoa wa Morogoro Mhandisi Benjamin Maziku kusimamia ukamilishaji wa mradi huo kwa muda uliopangwa na si vininevyo.
Aidha, amemuagiza Meneja huyo wa TARURA Mkoa wa Morogoro kuanza kufanya utafiti wa kufanyia matengenezo maeneo yasiyopitika kiurahisi barabara hiyo ambayo inaunganisha Wilaya ya Kilindi Mkoani Tanga ili yaboreshwe na daraja hilo kuwa na tija kwa wilaya nne za Kilosa na Gairo za Mkoa wa Morogoro na Kilindi na Handeni kwa Mkoa wa Tanga.
Waziri Bashungwa (wa pili kushoto) pamoja na ujumbe wake wakiangalia ujenzi wa Daraja jipya. Kushoto ni Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Martine Shigela, Kushoto kwake ni Mbunge wa Jimbo la Kilosa Prof. Mhe. Palamagamba Kabudi na kulia ni Kaimu Katibu Tawala Mkoa wa Morogoro, Mhandisi. Ezron Kilamhama.
Mwonekano wa ujenzi wa Daraja jipya la Belega.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Martine Shigela akifafanua kuhusu hatua zilizokwisha chukuliwa juu ya ujenzi wa shule ya sekondari ya Belega amesema zimeundwa timu mbili moja inahusika na ukaguzi (Auditing)kujiridhisha kama manunuzi ya vitendea kazi yalifuata kanuni na taratibu, kamati nyingine ni ile takayojikita upande wa utalaam wa uhandisi.
Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Martine Shigela wakifurahia jambo na Waziri Bashungwa, Kushoto ni Katibu wa CCM wilaya ya Kilosa.
Amesema timu zote hizo mbili zinatarajia kuanza kazi Julai 25 2022, na kwamba wajumbe wa kamati hizo watatoka TBA, TEMESA, National Housing, Wataalamu kutoka ngazi ya Mkoa pamoja na vyombo vya Ulinzi na Usalama.
Naye Mbunge wa Jimbo la Kilosa Mhe. Profesa Palamagamba Kabudi ameishukuru Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Mhe. Samia Suluhu Hassan kwa kuwezesha fedha za miradi hiyo jimboni kwake hususan ujenzi wa Daraja la Belega ambalo ni muhim sana kwa wananchi wa Kata ya belega kwani amesema daraja hilo limekuwa kero kwa wananchi wake kwa muda mrefu.
Waziri wa TAMISEMI Mhe. Innocent Bashungwa akipokea zawadi ya mbuzi kutoka kwa wakazi wa kata ya Nhembo, mara baada ya kukagua ujenzi wa kituo cha Afya cha Nhembo. Kulia ni Mbunge wa Jimbo la Kilosa Prof. Mhe. Palamagamba Kabudi, akishuhudia tukio hilo.
Huku Meneja wa TARURA Mkoa wa Morogoro Mhandisi Benjamin Maziku akibainisha kuwa mradi huo wa barabara unatekelezwa kwa miezi 18 kuanzia Disemba 21, 2021 uliposainiwa hadi Juni 20, 2023 na kwamba gharima ya mradi hadi kukamilika ni shilingi 7,905,122,445.65 (bila VAT) hadia na kwamba ujenzi wa daraja hadi sasa umefikia asilimia 13.7
Waziri Innocent Bashungwa akikamilisha ziara yake ya siku moja Wilayani Kilosa kwa kutembelea ujenzi wa Kituo cha Afya cha Nhembo kilichopo kata ya Mabula na kuwapongeza wananchi wa kata hiyo kwa kushiriki kikamirifu katika ujenzi wa kituo hicho cha Afya.
Waziri Bashungwa ampongeza mmoja wa wazee walioshiriki kikamilifu katika ujenzi wa kituo cha Afya Nhembo.
MWISHO
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Morogoro
Sanduku la Posta: S.L.P 650 MOROGORO
Simu: +2550232934305
Simu: +255766828252
Barua pepe: ras.morogoro@tamisemi.go.tz
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.