Waziri Zimbabwe akiri Tanzania ilijitoa mhanga wakati wa harakati za ukombozi wa Taifa lao
Waziri wa Habari na Utangazaji wa Jamhuri ya Zimbabwe Mhe.Monica Mtsvangwa amesema anatambua kuwa Tanzania ilitoa chango mkubwa kwa ukombozi wa nchi yao kutokana na kujitoa mhanga kwake kuwapatia mafunzo wapigania uhuru wa Zimbabwe Pamoja na kutenga maeneo kwa ajili ya kambi zao lengo ni kuhakikisha kuwa nchi ya Zimbabwe inapata uhuru wake.
Waziri wa Habari na Utangazaji wa Jamhuri ya Zimbabwe Mhe.Monica Mtsvangwa
Waziri Mtsvangwa ametoa kauli hiyo Disemba 18 mwaka huu Ofisini kwa Mkuu wa Mkoa wa Morogoro akiwa katika ziara ya siku moja Mkoani humo kwa ajili ya kukusanya taarifa na kumbukumbu za harakati za Ukombozi wa Zimbabwe zilizopo hapa nchini.
Amesema, Tanzania ilijitoa mhanga katika kutoa mafunzo kwa wapigania uhuru wa Zimbabwe Pamoja na kutoa maeneo mbalimbali ili kutoa fursa kwa wapigania uhuru hao kupata mafunzo ya mbinu za kuikomboa nchi yao, hivyo ameishukuru Tanzania kwa mchango huo huku akiomba kudumisha udugu na shirikiano huo baina ya nchi hizo mbili.
Mhe. Monica Mtsvangwa akipewa maelezo kutoka kwa Dkt. Salum Mwandu mara alipowasili katika eneo ambalo kulikuwa ni chuo cha madaktari
Akifafanua zaidi kuhusu ziara yake, amesema yupo hapa nchini kwa ajili ya kutembelea kambi hizo ambapo taarifa zake zitasaidia kutengeneza Makala maalum ya historia ya ukombozi wa taifa lao ambayo kwa namna moja ama nyingine imekosa muunganiko (gape) katika kueleza mfululizo wa histori ya ukombozi wa Taifa hilo hususan kwa kizazi cha sasa cha nchi hiyo.
Kwa upande wake kaimu Katibu Tawala wa Mkoa wa Morogoro Bw. Herman Tesha kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa huo Mhe. Martine Shigela amesema, ziara ya Waziri Monica Mtsvangwa inaonesha ushirikiano wa kihistoria uliopo baina ya nchi hizo mbili na kwamba ana Imani ziara hiyo itaimarisha zaidi mahusiano yaliyopo.
Waziri Monica Mtsvangwa akiteta jambo na mwenyeji wake Kaimu Katibu Tawala Mkoa wa Morogoro Bw. Herman Tesha (Katikati)
Aidha amesema, ziara ya Waziri Monica Mtsvangwa Mkoani Morogoro inaaksi upekee wa Mkoa wa Morogoro kuwa nao una mchango wa kipekee kuwa kitovu cha kambi mbalimbali za wapigania uhuru sio tu kwa nchi ya Zimbabwe bali pia kutoka nchi nyingine za kusini mwa bara la Afrika ikiwemo nchi ya Afrika ya Kusini.
Naye Mkurugenzi wa Maendeleo ya Utamaduni kutoka Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo Emmanuel Temu amesema Pamoja na kutunza maeneo ya kihistoria yaliyopo hapa nchini ambayo kwayo yanaipa heshima Tanzania, amewataka vijana hapa nchini kuiga uzalendo wa waasisi wa taifa hili kujitoa kwa ajili ya kupigania uhuru wa taifa la Tanzania na mataifa mengine Jirani.
“lengo kubwa ni kuhakikisha kuwa vijana wajifunze na kuiga uzalendo uliofanyika wakati huo” amesisitiza Bw. Emannuel Temu.
Mkurugenzi wa Maendeleo ya Utamaduni kutoka Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo Emmanuel Temu(kushoto) akijadiliana jambo na mwenyeji wakeambaye ni Kaimu Katibu Tawala wa Mkoa wa Morogoro Bw. Herman Tesha
Baadhi ya maafisa kutoka Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo wakipata maelezo kutoka kwa Dkt. Mwandu ambaye ni mwazilishi wa chuo hicho na wenzake watatu na kuhudumu kama Chief Academy. Kulia ni Mkurugenzi wa Maendeleo ya Utamaduni kutoka Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo Emmanuel Temu na kushoto ni Afisa Habari wa Wizara hiyo Bw, Eleuteri Mangi
Katika hatua nyingine Bw. Temu amesema kutokana na uzalendo na kujitoa mhanga kwa waasisi wa taifa hili akiwemo hayati Mwal. Julius Kambarage Nyerere kusaidia nchi nyingine kujikomboa kumesaidia kukubalika haraka wazo lililotolewa na Tanzania la kutaka kuwa na programu ya URITHI WA UKOMBOZI WA AFRIKA wazo ambalo Umoja wa Afrika umebariki na kazi hiyo imekwisha anza tangu mwaka 2011.
Haya ni baadhi ya majengo yaliyokuwa ya chuo cha Madaktari wa vyama vya ukombozi vya nchi zilizo kusini mwa Bara la Afrika kilichoitwa kwa jina la United Nations Health Assistance to Southern Afriacan Liberations Movement 1976 – 1985.
Akifafanua Zaidi Temu amesema, lengo la programu hiyo ambayo kwa sasa iko chini ya Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo ni kuhakikisha kuwa Wizara inatafuta, inatambua, inaendeleza, inatangaza na kuhifadhi urithi wote wa ukombozi uliopo hapa nchini.
Katika Ziara hiyo Waziri Mtsvangwa akiwa Mkoani Morogoro ametembelea eneo la kihistoria ambalo awali lilikuwa ni chuo cha kuandaa madaktari kutoka nchi ambazo zilikuwa hazijapata uhuru chuo kilichojulikana kwa jina la United Nations Health Assistance to Southern Afriacan Liberations Movement, chuo hicho kilichoanza mwaka 1976 hadi 1985.
Afisa Utamaduni wa Kituo cha Urithi wa Ukombozi wa Bara la Afrika Getrude Ndalo (mwenye suti ya rangi ya damu ya mzee) kutoka Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo akitoa maelezo mahusus kwa Mhe. Waziri
Kwa mujibu wa Dk.Salum Mwandu mmoja wa madaktari watatu waazilishi wa chuo hicho anasema, kilianzishwa kwa malengo mahususi ili kupata Madaktari wa vyama vilivyokuwa vimesajiliwa vya kupigania uhuru kwa nchi za kusini mwa Afrika ili nchi hizo zitakapojitawala ziweze kujitegemea katika sekta ya Afya lakini pia madaktari hao ndio walihusika kwa karibu kutoa huduma za kitabibu wakatika wote wa harakati za Ukombozi.
Dkt. Salum Mwandu miongoni mwa waazilishi watatu wa chuo hicho ambaye kwa sasa anafanya kazi zake katika hospitali ya binafsi hapa mjini Morogoro. wenzake ambao wote ni marehemu ni pamoja na Dkt John Kasiga aliyekuwa anawakilisha Umoja wa Afrika - OAU (wakati huo) na Dkt. Manto Tshabalala kwa niaba ya libaration movement
Vyama vya siasa vilivyoleta wanafunzi wao katika chuo hiki ni Pamoja na chama cha ZANU -PF Zimbabwe African National Union – Patriotic Front (Zimbabwe), ZAPU - Zimbabwe African People‘s Union (Zimbabwe), ANC - African National Congress (South Africa), SWAPO - South – West African People’s Organization (Namibia)na vyama vingine vingi.
Mhe. Waziri Monica Mtsvangwa tayari ametembelea eneo la kihistoria la Kongwa Mkoani Dodoma, ametembelea eneo lililokuwa chuo cha madaktari hapa Morogoro, ametembelea Kaole Bagamoyo Mkoani Pwani, na anatarajia kutembelea Kambi ya Wakimbizi ya Mgagao Mkoani Iringa na Nachingwea Mkoani Lindi maeneo ambayo pia wapigania uhuru kutoka Zimbabwe waliishi.
MWISHO
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Morogoro
Sanduku la Posta: S.L.P 650 MOROGORO
Simu: +2550232934305
Simu: +255766828252
Barua pepe: ras.morogoro@tamisemi.go.tz
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.